Kwako mpendwa uliyeanza safari ya wokovu, nimekuwekea mambo muhimu saba ya kufahamu kwamba yanatokea ndani yako automatically pindi tu unapompokea Yesu ndani yako. Soma haya na ufahamu wako ukapokee katika Jina la Yesu Kristo!

Anaandika Hosea Gambo, Mtumishi wa Mungu;
  1. Unafanyika mtoto wa Mungu (Mwana wa Mungu).

Jambo la kwanza kabisa na muhimu sana kutambua ukiishakumpokea Bwana Yesu ndani yako, ni kwamba umehamishwa family kiroho na kuingia katika familia ya Mungu, tena unakuwa umefanyika mwana wa Mungu. “Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake;” YOH. 1:12

Yesu Kristo akiingia ndani yako anakuwa ameingia kwa yule Roho mtakatifu. Alisema sintawaacha yatima, maana yake atabaki nasi lakini katika namna nyingine (1YOH. 3:24). Kwamaana hiyo akiwa ndani yetu, anakuwa anashuhudia pamoja na roho zetu. “Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu, ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu;” RUM. 8:16

  1. Unasamehewa dhambi zako zote (unafanyika mtakatifu).

Kabla ya wokovu, sisi wote tulikuwa watenda dhambi. Hatukufaa kitu mbele za Mungu wetu. Tumedumu katika kumchukiza Mungu. Lakini sasa kwa kitendo cha kumpokea Yesu Kristo ndani yetu, tunakuwa tumepokea msamaha wa dhambi/ondoleo la dhambi, tunakuwa tumeingiza ndani kitakatifu kisichoweza kukaa na uchafu wa aina yoyote. Kwa maana hiyo uchafu/dhambi zote zinatakasika na unakuwa mtakatifu. Biblia inasema; “Katika yeye huyo, kwa damu yake, tunao ukombozi wetu, masamaha ya dhambi, sawasawa na wingi wa neema yake.” EFE. 1:7

Nabii Yeremia aliutabiri wakati huu wa kumpokea Kristo na kwamba hatutakuwa na kazi kubwa ya kufundishana bali yeye aliye ndani yetu atakuwa na huo wajibu tena kwamaana tumefutiwa uovu wote. “Wala hawatamfundisha kila mtu jirani yake, na kila mtu ndugu yake, wakisema, Mjue Bwana; kwa maana watanijua wote, tangu mtu aliye mdogo miongoni mwao hata aliye mkubwa miongoni mwao, asema Bwana; maana nitausamehe uovu wao, wala dhambi yao sitaikumbuka tena.” YER. 31:34

  1. Unajazwa Roho wa Mungu (Roho Mtakatifu).

Nimeshasema hapo juu kwamba kuingia kwake ndani yetu na kukaa huko ni kwa yule Roho mtakatifu ambaye yeye mwenyewe alimfanya kuwa ahadi kwetu. Kwa hiyo ukimpokea Yesu ndani yako, unapokea kujazwa Roho mtakatifu. “Mkinipenda, mtazishika amri zangu. Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele; ndiye Roho wa kweli; ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa kuwa haumwoni wala haumtambui; bali ninyi mnamtambua, maana anakaa kwenu, naye atakuwa ndani yenu.” YOH. 14:15-17

Unapookoka kwa maana ya kumpokea Yesu Kristo ndani yako, unafanyika hekalu la Roho mtakatifu yaani hifadhi ya Roho mtakatifu. Biblia inasema; “Hamjui ya kuwa ninyi mmekuwa hekalu la Mungu, na ya kuwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu? Kama mtu akiliharibu hekalu la Mungu, Mungu atamharibu mtu huyo. Kwa maana hekalu la Mungu ni takatifu, ambalo ndilo ninyi.” 1 KOR. 3:16-17

  1. Umehamishwa kutoka mautini kwenye ufalme wa giza (wa shetani) na kuingizwa uzimani katika Ufalme wa Nuru (wa Mungu).

Nilisema kwamba katika ulimwengu wa Roho, kitendo cha kumpokea Bwana Yesu ni kufanya mapinduzi makubwa ya kiufalme. Ulikuwa umekaa katika ufalme mwovu wa shetani na sasa unakuwa umehamishwa na kuingizwa katika Ufalme wa Mungu. “Naye alituokoa katika nguvu za giza, akatuhamisha na kutuingiza katika ufalme wa Mwana wa pendo lake;” KOL. 1:13

Ufalme ambao tumetolewa ni ufalme wenye mauti kama thawabu yake, lakini kitendo hiki cha kimapinduzi katika maisha yetu katika ulimwengu wa Roho kinatuingiza katika ufalme wenye thawabu ya uzima wa milele. “Amin, amin, nawaambia, Yeye alisikiaye neno langu na kumwamini yeye aliyenipeleka yuna uzima wa milele; wala haingii hukumuni, bali amepita kutoka mautini kuingia uzimani.” YOH. 5:24

Kwa maana hiyo tumeingia katika ufalme wa upendo, tunapaswa kuishi katika kuitenda amri kuu ambao ni amri ya upendo. Biblia inasema hivi “Sisi tunajua ya kuwa tumepita toka mautini kuingia uzimani, kwa maana twawapenda ndugu. Yeye asiyependa, akaa katika mauti.” 1YOH. 3:14


  1. Jina lako sasa linakuwa limeandikwa katika Kitabu cha uzima cha Mwana-komdoo.

Kitendo kumpokea Yesu Kristo ndani yetu kinatupa usajili katika kitabu kikuu cha wana wa Mungu. Amini kwamba kama umeokoka hakika jina lako limeishaandikwa katika kitabu kile kitakatifu cha mwana kondoo. Yesu aliwaambia wanafunzi wake “Lakini, msifurahi kwa vile pepo wanavyowatii; bali furahini kwa sababu majina yenu yameandikwa mbinguni” LUK. 10:20. Tusiishie kuwa na furaha kwa mamlaka tuliyobeba tu kwamba miujiza inatendeka kwayo, bali furaha yetu iwe kwasababu ya majina yetu kuandikwa katika kitabu cha uzima huko mbinguni.

Hata Paulo mtume anatusihi kwamba tusaidiane sisi ambao tumeshaokoka, sisi ambao majina yetu yameshaandikwa katika kitabu cha uzima. “Naam, nataka na wewe pia, mjoli wa kweli, uwasaidie wanawake hao; kwa maana waliishindania Injili pamoja nami, na Klementi naye, na wale wengine waliotenda kazi pamoja nami, ambao majina yao yamo katika kitabu cha uzima.” FIL. 4:3

Usaji huu unatupa uwezo wa kuingia katika ufalme wa Mbinguni, kwa maan hakuna asiyeandikwa humo atakayeingia katika ufalme wa Baba. “Na ndani yake hakitaingia kamwe cho chote kilicho kinyonge, wala yeye afanyaye machukizo na uongo, bali wale walioandikwa katika kitabu cha uzima cha Mwana-Kondoo.” UFU. 21:27

(Unakuwa umesajiliwa kuwa mwana wa mbinguni)

  1. Umepewa mamlaka makubwa ya kufungua na kufunga, kukanyaga mamlaka ya giza.

Kitendo cha Yesu kuingia ndani yako na kukaa kwako kimekupa wewe mamlaka makubwa sana dhidi ya falme na utawala wote. Kwa jina la Yesu Kristo falme zote zinatii, katika Damu ya Yesu Kristo tumepokea nguvu ya utakaso na umiliki, tumepokea agano la milele agano lidumulo; katika Neno la Kristo tumebeba silaha nzito sana inayoweza kutengamanisha hata nafsi na roho; tunayo malka kwa yule Roho ambaye sasa anaishi ndani yetu. Hakika tumepokea uweza utokao juu. “Nami nitakupa wewe funguo za ufalme wa mbinguni; na lo lote utakalolifunga duniani, litakuwa limefungwa mbinguni; na lo lote utakalolifungua duniani, litakuwa limefunguliwa mbinguni.” MAT. 16:19

Tutatembea katika kukanyaga mitego, madhara na hatari lakini hatutapata madhara ya aina yoyote, tutalishwa kila aina ya sumu kwasababu aliye ndani yetu ni mkuu kamwe hatutapata madhara. Tunakuwa katika mstari wa wokovu kwa maana ya kutokudhurika. Biblia inasema “Tazama, nimewapa amri ya kukanyaga nyoka na nge, na nguvu zote za yule adui, wala hakuna kitu kitakachowadhuru.” LUK. 10:19

  1. Unakuwa na ulinzi thabiti wa malaika wa Mungu kila saa.

Kwasababu kitendo cha wewe kuokoka kinao umuhimu mkubwa sana katika ufalme wa Mbinguni; unapoamua kuokoka baraza la juu mbinguni linasimama kushangilia kwa furaha kubwa, Mungu anafurahia maamuzi yako ya ukombozi wako kwasababu anakupenda. Na ufalme wa giza kwasababu ya hila wanazidi katika kukutafuta, kwa maana hiyo unakuwa umeingia katika vita kubwa ya kiroho. Mungu anawatuma malaika wake, Biblia inasema wanaweka kituo kwako kukulinda. “Malaika wa Bwana hufanya kituo, Akiwazungukia wamchao na kuwaokoa.” ZAB. 34:7

Ukizidi kuhakikisha Bwana Yesu anakaa ndani yako, malaika wanakulinda katika kila sehemu maishani mwako; “Kwa kuwa atakuagizia malaika zake Wakulinde katika njia zako zote.” ZAB. 91:10-11