SIKU YA KWANZA:

TAR. 29/07/2019

(Semina ya mafundisho ya Neno la Mungu BIBLIA NI JIBU LAKO)


Ninayewasilisha mafundisho ya siku ya kwanza ni mimi Hosea Gambo Jnr, ni RAIS na MWASISI wa huduma hii ya BIBLIA NI JIBU.


Nawasalimu sana katika jina la Yesu Kristo!

Karibu katika siku ya kwanza ya semina ya Neno la Mungu na ujumbe tajwa hapo juu; kama kawaida kila mwisho wa mwezi tunapata hii fursa njema ya kupeana semina za namna hii kusudi NENO LA MUNGU KUJAA NDANI YETU SOTE.

Mafumdisho yangu yatakaa sana katika mstari wa kuonesha dhana ya kwanini huduma hii inaitwa BIBLIA NI JIBU LAKO na kwanini moto wake ni “Neno la Kristo likae kwa wingi ndani yako

…ambapo nitasimama katika andiko hili; ❝Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu katika hekima yote, mkifundishana na kuonyana kwa zaburi, na nyimbo, na tenzi za rohoni; huku mkimwimbia Mungu kwa neema mioyoni mwenu.
—Wakolosai 3: 16 (Biblia Takatifu)

YALIYOMO:

1. Utangulizi
2. Dhana ya huduma yetu
3. Nguvu 7 za Neno la Mungu ndani yako
4. Hitimisho


I. UTANGULIZI:

A) MADHUMUNI YA SOMO:

Madhumuni ya somo hili mpendwa mwana wa Mungu katika Kristo; kwanza kabisa ni kuimarisha nguvu ya kila mmoja aliyedhamiria kwa dhati ya moyo wake kuishi katika wokovu hata atakapoingia katika ule ufalme wa Baba. La pili ni kujenga uelewa juu ya huduma hii jinsi Mungu alivyoikusudia kuweka mwamko mioyoni mwetu. Na la tatu ni kukufanya msomaji uone jinsi ilivyo muhimu kuweka Neno la Mungu ndani yako ili kupata jawabu la maisha yako ya kiroho na kimwili.

B) NENO NI NINI?

Tunaanza na NENO; hii inamaanisha ujumbe wa aidha matamshi ya kitu chochote au maandishi. Ninasema matamshi ya kitu chochote kwasababu Biblia yangu inaniambia hata punda amesema neno. Biblia inasema hivi; ❝Bwana akakifunua kinywa cha yule punda, naye akamwambia Balaamu, Nimekutenda nini, hata ukanipiga mara tatu hizi?
—Hesabu 22: 28 (Biblia Takatifu)

Punda alisema NENO.

Lakini mara nyingi tumezoea ujumbe unao eleweka ni kutoka kwa mwanadamu; kumbe hata viumbe katika ulimwengu huu na ule wa roho pamoja na Mungu mwenyewe wanatupatia jumbe mbalimbali.

Twende kwenye lengo!

NENO katika Biblia; ni ujumbe wa Mungu maalum kwaajili yetu; Neno ni Mungu. Neno ni Yesu Kristo mwenyewe, aliye mwokozi wa maisha yetu.

Biblia inasema; ❝Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu.
—Yohana 1: 1 (Biblia Takatifu)

Kwa maana hiyo Biblia ipo wazi kwamba Neno ni Mungu. Biblia inasema tena; ❝Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli.
—Yohana 1: 14 (Biblia Takatifu)

Na hapa ndipo panapotuweka wazi kwamba Yesu Kristo ndiye Mungu na alikuja kweli katika mwili akaishi kama mwanadamu, naye alijitambulisha mwana wa Adamu ili katika hali hiyo atukomboe sisi tuliomezwa na dhambi hapo awali.

Biblia inasema tena; ❝Kisha nikaziona mbingu zimefunuka, na tazama, farasi mweupe, na yeye aliyempanda, aitwaye Mwaminifu na Wa-kweli, naye kwa haki ahukumu na kufanya vita. Na macho yake yalikuwa kama mwali wa moto, na juu ya kichwa chake vilemba vingi; naye ana jina lililoandikwa, asilolijua mtu ila yeye mwenyewe. Naye amevikwa vazi lililochovywa katika damu, na jina lake aitwa, Neno la Mungu.
—Ufunuo wa Yohana 19: 11-13 (Biblia Takatifu)

Huyu anayetambulishwa kama ndiye NENO LA MUNGU ni nani? Huyu ni Yesu Kristo mwana wa Mungu.

Neno ni roho; inapopenya ndani yako inaumbika na kukufanyia utu wa mwonekano wako. Neno la Mungu ni Roho ya Mungu; Roho ya Mungu ni Roho mtakatifu.

Tunaposema Neno ni Roho ni Biblia imesema hivyo; ❝Roho ndiyo itiayo uzima, mwili haufai kitu; maneno hayo niliyowaambia ni roho, tena ni uzima.❞
—Yohana 6: 63 (Biblia Takatifu)

II. DHANA YA HUDUMA HII YA BIBLIA NI JIBU LAKO:

Sisi tunaamini katika Biblia, na kwamba ni takatifu sana kuliko kitabu chochote kile.

Biblia ni Neno la Mungu lililohifadhiwa katika maandishi ili kutuongoza sisi kuijua kweli na kuishi katika kweli. Biblia ni takatifu kwasababu haina uwongo hata kidogo; kila Neno lililoandikwa humo ni KWELI na HAKIKA.

Takatifu maana yake ni isiyo na mawaa; isiyo na uchafu… Uchafu au mawaa katika Neno ni nini haswa? Ni uwongo na uzushi, Biblia siyo uwongo wala siyo uzushi; Biblia ni HAKIKA na KWELI.

Katika Biblia leo ndipo tunapata majibu ya kila kitu; imeandikwa muda mrefu uliopita ila tunapata majibu ya magonjwa yetu, shida na tabu zetu, mizigo ya dhambi; maswali ya ufahamu yanapata majibu, katika ulimwengu wa roho napo Biblia inatupa jibu…. Hakika BIBLIA NI JIBU LAKO.

Uwe unaumwa BIBLIA NI JIBU LAKO, uwe yatima BIBLIA NI JIBU LAKO; uwe wa kukata tamaa BIBLIA NI JBU LAKO, uwe hauna furaha na raha ya maisha BIBLIA NI JIBU LAKO, uwe na shida yoyote BIBLIA NI JIBU LAKO.

Biblia ni NENO LA MUNGU. Yesu Kristo ni Mungu. Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yetu sote.

Neno likikaa ndani yako; Yesu Kristo amekaa ndani yako, Mungu Baba amekaa ndani yako, Roho mtakatifu naye ndo amekaa mdani yako; kama utatu wote wa Mungu umekaa ndani yako, tayari umepata jawabu la haja zako

Pale unapookoka kwa maana kwamba unapompokea Yesu Kristo kuwa Bwana na mwokozi wa maisha yako; on spot unakuwa umeweka Neno ndani yako. Kinachofuata sasa baada ya hapo ni wewe kulitunza na kulishibisha Neno lililopo ndani yako.

Na namna sahihi ya kufanya hivyo ni kudumu katila kusoma Neno la Mungu na kulitii yaani kufanya kama linavyoagiza.

Neno linaagiza tudumu katika maombi, tutoe zaka na sadaka pamoja na matoleo yote, tuwe na imani, tulinde utakatifu na tusitende dhambi, tuwajali wasiojiweza, tupendane na tushirikiane nk nk.

Kumbe Neno la Mungu ndani yako inaleta NGUVU. Nguvu ni uwezo na mamlaka. Yaani ndani yako upo uwezo na mamlaka.

Sasa dhumuni la semina hii ni wewe mpendwa kutambua Nguvu ya Neno la Mungu ndani yako. Neno la Mungu limejaa mafumdisho, mausia, maonyo na namna ya kuishi haswa; Biblia inasema; ❝Kwa ajili hii mpende Bwana, Mungu wako, na kushika sikuzote mausia yake, na amri zake, na hukumu zake, na maagizo yake.
—Kumbukumbu la Torati 11: 1 (Biblia Takatifu)

Basi kumbe hapa tunapokaa katika Neno la Kristo tunakuwa tayari tunaitwa wanafunzi wa Yesu…. ❝Basi Yesu akawaambia wale Wayahudi waliomwamini, Ninyi mkikaa katika neno langu, mmekuwa wanafunzi wangu kweli kweli;
—Yohana 8: 31 (Biblia Takatifu)

III. NGUVU SABA ZA NENO LA MUNGU NDANI YAKO:

Maana Neno la Mungu li hai, tena lina nguvu, tena lina ukali kuliko upanga uwao wote ukatao kuwili, tena lachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, na viungo na mafuta yaliyomo ndani yake; tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo.
—Waebrania 4: 12 (Biblia Takatifu)

Biblia inasema; Neno la Mungu li hai; tena lina nguvu… Kwa mantiki tunapoliweka Neno ndani yetu tunapokea nguvu kubwa…. Na sasa tunakwenda kuangalia nguvu saba ambazo tunazipokea kutoka Neno la Mungu ndani yetu.

1) Nguvu ya uzima:

Neno la Mungu ndani yako limetia uzima tena ule wa milele; Biblia inasema; ❝Roho ndiyo itiayo uzima, mwili haufai kitu; maneno hayo niliyowaambia ni roho, tena ni uzima.
—Yohana 6: 63 (Biblia Takatifu)

Kama Neno ni Roho tena ni uzima; maana yake Neno ndani yako ni uzima ndani yako.

Sisi tuliopokea Neno la Mungu tumekea nguvu ya uzima. Uzima huu tumeupokea pale tulipookoka; maana Neno ni Yesu Kristo, kumpokea yeye ni kupokea Neno. Sasa tunao uzima ndani yetu katika Neno.

2) Nguvu ya majibu ya maombi yetu:

Biblia inasema hivi, ❝Ninyi mkikaa ndani yangu, na maneno yangu yakikaa ndani yenu, ombeni mtakalo lote nanyi mtatendewa.
—Yohana 15: 7 (Biblia Takatifu)

Yesu anatupa fursa ya upendeleo mkubwa; ni kwasababu Neno la Kristo tulimeliachilia ndani yetu. Sasa anatuambia hivi, kama Neno limekaa ndani yetu katika hekima yote basi tuombe lolote naye anatutendea.

Eneo la maombi linawafanya watu wengi wapwndwa kurudi nyuma; wamekaa katika maombo miaka nenda miaka rudi; lakini majawabu ya maombi yao hakuna… Kumbe kuna kitu kidogo tu!

Neno la Mungu halipo ndani yao. Wamepokea lakini hawajamwagilia… Namna sahihi ya kulimwagilia na kuliendeleza Neno la Mungu ndani yako ni kusoma Neno la Mungu, Biblia takatifu na si vinginevyo. Kwa kutimiza hilo tambua sasa tayari maombi yako yamepata majibu. Weka Neno la Mungu ndani yako katika bidii sana.

Ndiyo maana Mungu anamwagiza Yoshua wa Nuni, anasema; ❝Kitabu hiki cha torati kisiondoke kinywani mwako, bali yatafakari maneno yake mchana na usiku, upate kuangalia kutenda sawasawa na maneno yote yaliyoandikwa humo; maana ndipo utakapoifanikisha njia yako, kisha ndipo utakapositawi sana.
—Yoshua 1: 8 (Biblia Takatifu)

Alimwagiza kusoma Torati kila wakati; mchana na usiku inamaana masaa 24. Na aliweka bayana kwamba, ndipo utakapofanikisha njia yako, kisha ndipo utasitawi sana.

3) Nguvu ya kumulika njia zetu:

Biblia inasema hivi… ❝Neno lako ni taa ya miguu yangu, Na mwanga wa njia yangu.❞
—Zaburi 119: 105 (Biblia Takatifu)

Neno linatupa nguvu ya kusafisha njia zetu; kwa maana kwamba inatufanya tusiweze kutenda dhambi. Usafi wa njia hautakufanya ujikwae… Kujikwaa ni kuingia dhambini.

Ukiliweka Neno la Mungu ndani yako, jua kwamba umeweka Nguvu ya ushindi dhidi ya dhambi; ❝Moyoni mwangu nimeliweka neno lako, Nisije nikakutenda dhambi.
—Zaburi 119: 11 (Biblia Takatifu)

Mahala hapa kwenye Zaburi ndipo pananifanya nione nguvu ya kuishinda dhambi kwamba ipo ndani yangu; Biblia inasema… ❝Jinsi gani kijana aisafishe njia yake? Kwa kutii, akilifuata neno lako.
—Zaburi 119: 9 (Biblia Takatifu)

Mpendwa mwana wa Mungu; acha nikwambie kitu….

Ukiweka ndani yako Neno la Mungu; hakikisha hilo Neno unalienseleza… Soma kwa bidii Biblia yako maana ni jibu lako. Na kama Neno ukiliendeleza jua kwamba umeweka hazina ya nguvu ushindi dhidi ya dhambi.

4) Nguvu ya Imani:

Kwanza kabisa hapa utambue kwamba chanzo cha Imani ni nini… ❝Basi imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo.
—Warumi 10: 17 (Biblia Takatifu)

Ukilisikia Neno la Mungu; mtumishi mmoja alinifundisha hapa kwamba kusikia ni kutii… Ukilitii Neno la Kristo, ujue kwamba umeweka ndani yako Nguvu ya Imani.

Habari fulani ya wanafunzi wa Yesu, pale walipokuwa wanavuka kwenda ng’ambo wakiwa na chombo inanionesha wazi kwamba chanzo cha imani ni kusikia Neno la Kristo. Biblia inasema; ❝Akawaambia, Mbona mmekuwa waoga? Hamna imani bado?
—Marko 4: 40 (Biblia Takatifu)

Yesu anawauliza hamna imani bado??? Maana wamepungukiwa nguvu ya Neno. Pale Yesu alipowaambia hivi ….Na tuvuke mpaka ng’ambo.❞
—Marko 4: 35 (Biblia Takatifu)

Hawakusikia hilo Neno ndiyo maana hawakuwa na Imani. Wangeweza kusikia hilo Neno basi wangekuwa na Imani.

Hii habari ya Petro pia inanifundisha dhahiri kwamba huyu sasa alikuwa na imani lakini alitakiwa awe na nguvu zaidi… ❝Lakini alipouona upepo, akaogopa; akaanza kuzama, akapiga yowe, akisema, Bwana, niokoe.
—Mathayo 14: 30 (Biblia Takatifu)

Petro alikuwa na ujuzi kwamba Imani chanzo chake ni kusikia Neno la Kristo; hivyo alilitaka hilo Neno kwanza, ❝Petro akamjibu, akasema, Bwana, ikiwa ni wewe, niamuru nije kwako juu ya maji.
—Mathayo 14: 28 (Biblia Takatifu)

Mara Yesu aliposema Neno naye akatii; ❝Akasema, Njoo. Petro akashuka chomboni, akaenda kwa miguu juu ya maji, ili kumwendea Yesu.
—Mathayo 14: 29 (Biblia Takatifu)

Nguvu ya Neno ndani yako ni UIMARA WA IMANI YAKO… Hatakama ukipotishwa kwenye dhoruba namna gani utakuwa imara tu!

5) Nguvu ya Kuumba:

Imeandikwa katika Biblia; ❝Kwa imani twafahamu ya kuwa ulimwengu uliumbwa kwa neno la Mungu, hata vitu vinavyoonekana havikufanywa kwa vitu vilivyo dhahiri.
—Waebrania 11: 3 (Biblia Takatifu)

Neno la Mungu liliumba ulimwengu huu na vitu vyote ikiwemo mimi na wewe. Neno lina nguvu ya kuumba!

Kwa neno la Bwana mbingu zilifanyika, Na jeshi lake lote kwa pumzi ya kinywa chake…. Maana Yeye alisema, ikawa; Na Yeye aliamuru, ikasimama.
—Zaburi 33: 6, 9 (Biblia Takatifu)

Hapa tunaona neno lilivyo na nguvu katika uumbaji. Mungu aliumba kila kitu kwa Neno lake tu.

Sisi katika Yohana 10:35 Biblia inasema tu miungu wadogo… ❝Yesu akawajibu, Je! Haikuandikwa katika torati yenu ya kwamba, Mimi nimesema, Ndinyi miungu?
Ikiwa aliwaita miungu wale waliojiliwa na neno la Mungu; (na maandiko hayawezi kutanguka);
—Yohana 10: 34-35 (Biblia Takatifu)

Kama ndivyo, kwamba sisi tu miungu, basi nasi tumepewa haya mamlaka ya uumbaji katika ndimi zetu kama Neno lipo ndani yetu…

Matamshi ya midomo yetu tuichunge saana. Yakobo alitamkiwa Baraka na babaye Isaka, na akabarikiwa sana. Tunafahamu hata akiwa ugenini akiwa anachunga mbuzi na kondoo, wakwake walizaa sana.

Kwasababu Neno lina nguvu ya kuumba, wana wa Mungu tujifunze kusema baraka midomoni mwetu badala ya laana na mikosi. Tuepushe mibalaa kwa Nguvu ya Neno ya kuumba; na kila wema, kweli na haki ni Neno la Mungu daima.

Nabii Ezekiel anatutaka tuwe manabii katika maisha yetu, nasi tutakuwa hivyo kama tutatambua nguvu ya Neno iliyopo ndani yetu katika wokovu. ❝Ndipo akaniambia, Tabiri, utabirie upepo, mwanadamu, ukauambie upepo, Bwana MUNGU asema hivi; Njoo, kutoka pande za pepo nne, Ee pumzi, ukawapuzie hawa waliouawa, wapate kuishi.
—Ezekieli 37: 9 (Biblia Takatifu)

Alitumia vyema nguvu ya Neno ya kuumba hata majeshi yalikufa yakapokea uhai…. Ameeen!

6) Nguvu ya Kuponya!

“Yesu akamwambia, “Nitakuja kumponya.” Huyo jemadari akamwambia, “Bwana, sistahili uingie nyumbani mwangu. Lakini sema tu neno, na mtumishi wangu atapona. Kisha Yesu akamwambia huyo jemadari Mroma, “Nenda nyumbani; na iwe kama ulivyoamini.” Na mtumishi wake akapona saa ileile.” Mathayo 8:7‭-‬8‭, ‬13 BHN.

Huyu jemadari alitambua nguvu ya Neno katika kuponya; alisema …tamka tu Neno na mtumishi wangu atapona.

Soma na haya maandiko mtumishi mpendwa wa Mungu; “Kulikuwa na mtu mmoja huko Lustra ambaye alikuwa kiwete tangu kuzaliwa, na alikuwa hajapata kutembea kamwe. Mtu huyo alikuwa anamsikiliza Paulo alipokuwa anahubiri. Paulo alimtazama kwa makini, na alipoona kuwa alikuwa na imani ya kuweza kuponywa, akasema kwa sauti kubwa, “Simama wima kwa miguu yako!” Huyo mtu aliyelemaa miguu akainuka ghafla, akaanza kutembea.” Matendo 14:8‭-‬10 BHN.

Tumeona Bwana Yesu anaambiwa na huyo Jemadari, TAMKA NENO NAYE ATAPONA!!!! Labda unaweza sema kwamba Yesu siyo mimi na wewe… Lakini pia Petro akamsimamisha kiwete na kumwaru atembee kwa NENO TU! Huyu sasa anatambua nguvu ya Neno ndani yake kwamba inaleta uponyaji.

Tambua kwamba ndani yako likiwemo Neno basi una nguvu ya kuponya. Weka Neno la Mungu ndani yako mpendwa.

7) Nguvu ya kumshinda mwovu:

Biblia inatuambia kwamba, “Tena ipokeeni chapeo ya wokovu, na upanga wa Roho ambao ni neno la Mungu;” Waefeso 6 :17

Unapokuwa na neno la Mungu na ukilitumia katika maombi, mwovu shetani anakuona umebeba upanga mkali sana wakutisha hakika…

Neno hukata kuwili, halibakizi hata kidogo. Sisi tunatumia Neno kama silaha katika vita ya ulimwengu wa roho. Ili tuweze kuwa na maisha ya ushindi katika wokovu, lazima kuwa na hii silaha nzito.

Hii ndiyo nguvu ya Neno la Mungu; kwamba inamshinda mwovu; ❝Nao wakamshinda kwa damu ya Mwana-Kondoo, na kwa neno la ushuhuda wao; ambao hawakupenda maisha yao hata kufa.
—Ufunuo wa Yohana 12: 11 (Biblia Takatifu)

Tunajifunza haya kwa Yesu Kristo wa Nazareth; alipokuwa katika kujaribiwa alitumia Neno… Alikuwa anatufundisha kwamba imo nguvu katika Neno na namna ya kufanya ili kumshinda mwovu; ❝Ndipo Yesu alipomwambia, Nenda zako, Shetani; kwa maana imeandikwa, Msujudie Bwana Mungu wako, umwabudu yeye peke yake. Kisha Ibilisi akamwacha; na tazama, wakaja malaika wakamtumikia.
—Mathayo 4: 10-11 (Biblia Takatifu)

Yesu akamwambia hivi; imeandikwa…. Maana yake ipo kwenye Biblia Neno la Mungu!

IV. HITIMISHO:

Kila andiko, lenye pumzi ya Mungu, lafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza, na kwa kuwaadibisha katika haki;
—2 Timotheo 3: 16 (Biblia Takatifu)

Tunaona kuwa kila andiko lililoko kwenye Biblia lina pumzi ya Mungu. Maana kwamba ni Neno kamili la Mungu aliye hai.

Mungu alisema nasi; alisema na kila mmoja mwenye mwili kwasababu kuu tatu;

1. Kutufundisha sisi.
2. Kutuonya sisi katika njia sahihi.
3. Kutuadabisha sisi.

Neno la Mungu, ni HAKIKA na KWELI. Haina shaka hata kidogo. Nasi tunapaswa kuamini kila andiko kama lilivyo. Kila andiko linatufaa kwa ile namna tatu hapo juu.

Tunapaswa kuwa wasomaji wa Neno la Mungu. Neno la Mungu linapaswa kukaa mioyoni mwetu, na tunapaswa kutembea katika Neno la Mungu. Tunapaswa kuliishi neno la Mungu!

Biblia inasema ❝Jinsi gani kijana aisafishe njia yake? Kwa kutii, akilifuata neno lako.
—Zaburi 119: 9 (Biblia Takatifu)

Daudi aliyatamka haya maandiko; “Moyoni mwangu nimeliweka neno lako, Nisije nikakutenda dhambi. Ee Bwana, umehimidiwa, Unifundishe amri zako.” Zaburi 119 :11-12

Daudi alizidi kusema maneno ya Mungu kwamba ; “Nitayatafakari mausia yako, Nami nitaziangalia njia zako. Nitajifurahisha sana kwa amri zako, Sitalisahau neno lako.” Zaburi 119 :15-16

Daudi anatuambia jambo la msingi sana… NI JINSI GANI KIJANA AISAFISHE NJIA YAKE? ….Kwa kutii, AKILIFUATA NENO LA MUNGU! Hauwezi kulifuata Neno la Mungu kama halijakaa moyoni mwako, kama hujashiba Neno… Maana utakuwa hulijui… Lakini pia hauwezi kuliweka Neno moyoni kama si msomaji waNeno la Mungu….

Ni muhim sana kulisoma Neno kwa nguvu zoteeee ili kuliweka moyoni, na kuliishi kwa kulifuata.

Daudi anasema nimeliweka Neno la Mungu moyoni… Hivyo hawezi kutenda dhambi! Kumbe ukilishiba neno la Mungu, unakuwa mgumu kwenye kutenda dhambi…

Neno linakuepusha na dhambi kwakweli; hili linakuwa pale unapotembea katika Neno, unapoliishi Neno au unapotenda sawasawa na Neno la Mungu! Daudi anamhimiza Bwana amfundishe amri zake… Kama unampenda Mungu/Yesu sharti uzishike na kuzitenda mari zake.

Amri za Mungu, ni Neno la Mungu…

Tunaweza tu kulisoma na kuliweka aneno na kulitenda siyo kwa uwezo wetu binafsi, sisi hatuwezi chochote bila Mungu mwenyewe…Tunahitaji kumtumaini Mungu.

Naweza kulisoma Neno, kuliweka moyoni, na kulitenda kwa msaada wa Mungu kupitia kwa Roho mtakatifu. Mausia ya Mungu yanapatikana katika Neno lake, njia za Mungu zipo kwenye Neno lake, uongozi wa Mungu upo kwenye Neno lake…

Hatimaye tunaona Daudi anasema, “sintalisahau neno la Mungu.” Yaani litamkaa moyoni…Unajua Neno likiisha kukaa moyoni unakuwa na uweza wa kulitenda. Sasa hapa unakuwa na uweza mkubwa wa kutembea katika Neno, kuishi katika Neno, kujaa Neno mdomoni…

Biblia inasema; “Lakini iweni watendaji wa neno, wala si wasikiaji tu, hali mkijidanganya nafsi zenu. Kwa sababu mtu akiwa ni msikiaji wa neno tu, wala si mtendaji, mtu huyo ni kama mtu anayejiangalia uso wake katika kioo. Maana hujiangalia, kisha huenda zake, mara akasahau jinsi alivyo. Lakini aliyeitazama sheria kamilifu iliyo ya uhuru, na kukaa humo, asiwe msikiaji msahaulifu, bali mtendaji wa kazi, huyo atakuwa heri katika kutenda kwake.” Yakobo 1 :22-25

Hapa Yakobo anaandika neno la Mungu ili nasi tusome na kujifunza, tupate adabu na tuaswe nalo. Yakobo ni njia ya Neno la Mungu… Anayesema nasi ni Mungu!

Iweni watendaji, siyo wasikilizaji!!!!

Ukiwa msikilizaji tu, utakosea sana maana utakuwa unajidanganya!
Biblia inasema kama utakuwa msikilizaji, ukaweza kuliweka nenot moyoni katika kumbukumbu zako, ukawa mtendaji… UTAKUWA NA HERI KATIKA UTENDAJI WAKO

Kumbe unaweza kulisoma Neno la Mungu, ukaliweka moyoni… Aidha umeelewa ama hujaelewa, na UKAWA SIYO MTENDAJI WA HILO NENO… Maana yake ni unatangaziwa “OLE”.

Hakuna binadamu aliye mkamilifu, wote ni watenda dhambi… Hata kama umeokoka, unaweza kutenda dhambi… Sioni shaka yoyote. Lakini unaweza kukaa katika kutokutenda dhambi, haswa kama umeokoka. Na maanisha, siyo kila wakati unatenda dhambi… Kuna nyakati tunakuwa watakatifu kabla ya miili kuishinda roho zetu.

Biblia ndiyo inasema “bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote;” 1 Petro 1:15

Ukishiba Neno la Mungu, unao uwezo mkubwa wa kukaa katika utakatifu haswa unapokuwa unaliishi. Tunaposema unaliishi Neno tunamaanisha… Mfumo mzima wa maisha yako unautiisha katika maandiko matakatifu, hautakosea kama unatenda sawasawa na Neno…

Usikose siku ya pili ya mafundisho haya kesho tar. 30/07/2019.

MUNGU AWABARIKI SANA!