Na Hosea Gambo

Jambo la kwanza

Kuomba katika jina la Yesu Kristo.


Biblia inasema hivi, “…Amin, amin, nawaambia, Mkimwomba Baba neno lo lote atawapa kwa jina langu.” YN. 16:23 SUV …

zingatia maneno “KWA JINA LANGU”, anayezungumza hapo ni Yesu Kristo.

Ili maombi yetu yajibiwe, tunapaswa kuomba katika jina la Yesu Kristo.

Kwanini tuombe kwa hilo jina?

Yesu Kristo ametupa mamlaka ya kutumia jina lake kwa maana kwamba tunapotumia jina lake tunakuwa tunasimama katika mahala pake.

Na kwasababu tumekuwa wa Kristo, tunapaswa kuishi katika Kristo, kuongea katika Kristo, kula katika Kristo, kuvaa katika Kristo, kuomba katika Kristo, … yote katika mamlaka ya Kristo iliyo juu yetu.

Maandiko yanasema, “Na kila mfanyalo, kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote katika jina la Bwana Yesu, …” KOL. 3:17 SUV

Kwa hiyo unapoomba katika jina la Yesu Kristo, kwasababu katika jina hilo unakuwa umebeba mamlaka ya Kristo; inakuwa siyo wewe tena bali Kristo mwenyewe anaomba, …ndiyo maana lazima ujibiwe.

Kumbuka tumefanyika wana wa Mungu kwaajili ya Kristo Yesu!

Jambo la pili

Kuomba katika Neno la Mungu.

Maandiko yanasema, “Mungu huliangalia Neno lake apate kulitimiza” …Mungu anatenda sawasawa na Neno lake, hatendi nje na Neno lake.

Kila kitu Mungu hufanya kwa kuzingatia Neno lake.

Kwahiyo unaona namna Neno la Mungu ni muhimu kwaajili ya maombi yako kujibiwa ipasavyo.

Kwanini tunapaswa kuomba sawasawa na Neno la Mungu?

…ni kwasababu Neno la Mungu ni chanzo cha imani.

Pasipo Neno la Mungu hapana imani.

Biblia inasema “Basi, Imani ni kuwa na hakika na mambo yatarajiwayo, ni bayana ya mambo yasiyoonekana.” EBR 11:1 SUV.

Inasema tena Biblia kwamba, “Basi imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la Kristo.” RUM. 10:17 SUV

Pasipo imani maombi hayajibiwi, na imani tunaipata katika Neno la Mungu.

Ndiyo maana tunasema hapa, na tunahubiri mno, Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yako…

Ni tunamaanisha kabisa kwa dhati kwamba pasipo Neno ndani yako hapana uhai kiroho!

Jambo la tatu

Kuomba kwa nguvu za Roho mtakatifu.


Tumepewa Roho mtakatifu ili awe msaidizi wetu, na katika mambo yametajwa atusaidie ni kwenye maombi, kwasababu hatujui namna ipasavyo kuomba.

Roho mtakatifu anatuongoza namna nzuri ya kuomba mbele za Mungu.

Yeye hutukumbusha mambo ya msingi na namna ya kuumba ombi kwa Mungu.

Huyu hutupa ujasiri wa kutamka hata maneno tusiyoweza kuyatamka kawaida.

Roho mtakatifu anaijua vzuri lugha ya kiroho ambayo ulimwengu wa kiroho huielewa zaidi.

Lugha hiyo sisi hatuijui kabisa.

Hivyo ili maombi yapate kujibiwa sawasawa yatupasa kuomba katika Roho mtakatifu.

Ukisoma katika Matendo ya mitume utagundua wale mitume wa Yesu walifanikiwa sana kiroho kwasababu walizingatia mambo haya makuu matatu katika kuomba kwao.

Mwana wa Mungu, nakukumbusha leo…

Omba kwa kuzingatia mambo haya, hakika yako utafanikiwa sana katika maisha yako kiroho hata kimwili, utafanikisha njia zako, utabarikiwa sana na hatimaye utaupokea urithi ule wa milele!