ROHO MTAKATIFU DAY THREE

Anawasilisha Mwlm. Peter Francis

BIBLIA NI JIBU LAKO

Roho Mtakatifu ni nani?

Roho Mtakatifu ni Mungu mwenyewe. Mungu wetu ni wa kanuni yupo katika utatu; Mungu baba, Mwana na Roho Mtakatifu. Leo nitazungumzia huyu mmoja ambaye ni Mungu Roho Mtakatifu.

Roho Mtakatifu Anakaa Wapi?

Roho Mtakatifu anakaa ndani ya Mtu. Mwanzo 41:38; “Farao akawaambia watumwa wake, Tupate wapi mtu kama huyu, mwenye roho ya Mungu ndani yake?”

Tunamwona Roho Mtakatifu anakaa ndani ya Mtu

Swali la kujiuliza kwanini anakaa ndani ya mtu? Inamaana amekosa pa kwenda?

Roho Mtakatifu anakaa patakatifu, kwahiyo ili akae ndani ya mtu sharti awe mtakatifu huyo Mtu. Roho Mtakatifu anakaa kwa waliookoka tu, hawezi kukaa kwa wasiookoka. Bila kuokoka utamsikia tu Roho Mtakatifu kwa watu wakimsema.

Sifa Na Kazi Za Roho Mtakatifu:

  • Hutujulisha yajayo kupitia ndoto

Ayubu 33:14-19; “Kwa kuwa Mungu hunena mara moja, Naam, hata mara ya pili, ajapokuwa mtu hajali. Katika ndoto, katika maono ya usiku, Usingizi mzito uwajiliapo watu, Katika usingizi kitandani; Ndipo huyafunua masikio ya watu, Na kuyatia muhuri mafundisho yao, Ili amwondoe mtu katika makusudio yake, Na kumfichia mtu kiburi; Yeye huizuia nafsi yake isiende shimoni, Na uhai wake usiangamie kwa upanga. Yeye hutiwa adabu kwa maumivu kitandani mwake, Na kwa mashindano yaendeleayo daima mifupani mwake;”

Roho Mtakatifu anatupa habari za yale yatarajiwayo kutupata mabaya au mazuri. Unaweza ukaota ndoto mbaya ya hatari ukapuuzia kabisa na usichukue hatua ukaja ukaumia kabisa

  • Tunajifunza kuwa Roho Mtakatifu anakuletea habari za mambo yanayotarajia kukupata katika ulimwengu wa mwili (ulimwengu wa macho).
  • Kutafsiri ndoto siyo kazi ya mtu ni kazi ya Roho Mtakatifu anayekaa ndani ya mtu

“Basi mwanadamu wa tabia ya asili hayapokei mambo ya Roho wa Mungu; maana kwake huyo ni upuzi, wala hawezi kuyafahamu, kwa kuwa yatambulikana kwa jinsi ya rohoni. Lakini mtu wa rohoni huyatambua yote, wala yeye hatambuliwi na mtu.” 1 Wakorintho 2:14-15 SUV

Bila Roho Mtakatifu mtu hawezi kuyatafsiri mambo ya rohoni akayaelewa. Kwa mfano Nebkadreza mfalme wa babeli alishindwa kutafsiri ndoto kwa sababu hakuwa na roho Mtakatifu ndani yake; Lakini kijana mdogo sana Daniel aliweza kutafsiri ndoto ya Mfalme kwasababu alikuwa na Roho Mtakatifu.

“Lakini Mungu ametufunulia sisi kwa Roho. Maana Roho huchunguza yote, hata mafumbo ya Mungu. Maana ni nani katika binadamu ayajuaye mambo ya binadamu ila roho ya binadamu iliyo ndani yake? Vivyo hivyo na mambo ya Mungu hakuna ayafahamuye ila Roho wa Mungu. Lakini sisi hatukuipokea roho ya dunia, bali Roho atokaye kwa Mungu, makusudi tupate kuyajua tuliyokirimiwa na Mungu. Nayo twayanena, si kwa maneno yanayofundishwa kwa hekima ya kibinadamu, bali yanayofundishwa na Roho, tukiyafasiri mambo ya rohoni kwa maneno ya rohoni.” 1 Wakorintho 2:10-13 SUV

  • Nguvu ya kuyatafsiri maandiko matakatifu ipo ndani ya Roho Mtakatifu ndani ya mtu.

Bila ROHO Mtakatifu utakuwa unaisoma biblia huielewi kabisa na wakati mwingine ukiishika tu unakamatwa na usingizi. Wapo watu waliookoka mkianza kujadili maandiko kila mtu aseme alichokielewa wanalimbia kabisa

Hata ukituma hapa mstari kila mtu aseme alichokielewa utaona ni wachache sana watakaotoa maoni

Kama unaamini Roho Mtakatifu anakupa siri za Mungu kuanzia leo ukitaka kusoma mwambie akufundishe kutafsiri usitegemee akili zako utashindwa na utaumiza kichwa na mwishowe utapotosha. Roho Mtakatifu ni mwalimu

  • Roho Mtakatifu anampatia mtu upako

Isaya 61:1; “Roho ya Bwana MUNGU i juu yangu; kwa sababu Bwana amenitia mafuta niwahubiri wanyenyekevu habari njema; amenituma ili kuwaganga waliovunjika moyo, kuwatangazia mateka uhuru wao, na hao waliofungwa habari za kufunguliwa kwao.”

Luka 4:18; “Roho wa Bwana yu juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona tena, Kuwaacha huru waliosetwa,”

Upako uliopewa na Roho Mtakatifu utumie kukomboa waliofungwa na ibilisi. Mtu aliyejaa upako wa Roho Mtakatifu anaamri juu ya pepo, na magonjwa. Mtu aliyejaa upako waovu humkimbia na wakimwona kwa mbali hutetemeka

Yesu alipokuwa amejaa upako kwa alifanya makuu mengi na alimkemea shetani kwa ujasiri na shetani alikimbia. Vivyo hivyo na mtu aliyejaa upako waovu humkimbia na kuanza kusemezana achana na huyo mlokole.

Matendo ya Mitume 10:38; “Habari za Yesu wa Nazareti, jinsi Mungu alivyomtia mafuta kwa Roho Mtakatifu na nguvu naye akazunguka huko na huko, akitenda kazi njema na kuponya wote walioonewa na Ibilisi; kwa maana Mungu alikuwa pamoja naye.”

Mtu akiwa na upako hata mapepo humwuliza unataka ututoe tuende wapi?

“Naye aliposhuka pwani, alikutana na mtu mmoja wa mji ule, mwenye pepo, hakuvaa nguo siku nyingi, wala hakukaa nyumbani, ila makaburini. Alipomwona Yesu alipiga kelele, akaanguka mbele yake, akasema kwa sauti kuu, Nina nini nawe, Yesu, Mwana wa Mungu aliye juu? Nakusihi usinitese. Kwa kuwa amemwamuru yule pepo mchafu amtoke mtu yule. Maana amepagawa naye mara nyingi, hata alilindwa kifungoni na kufungwa minyororo na pingu; akavikata vile vifungo, akakimbizwa jangwani kwa nguvu za yule pepo. Yesu akamwuliza, Jina lako nani? Akasema, Jina langu ni Jeshi; kwa sababu pepo wengi wamemwingia. Wakamsihi asiwaamuru watoke kwenda shimoni. Basi, hapo palikuwa na kundi la nguruwe wengi wakilisha mlimani; wakamsihi awape ruhusa kuwaingia wale. Akawapa ruhusa. Pepo wakamtoka mtu yule wakawaingia nguruwe, nalo kundi lilitelemka gengeni kwa kasi, wakaingia ziwani, wakafa maji. Wachungaji walipoona lililotokea walikimbia, wakaieneza habari mjini na mashambani.” Luka 8:27-33

Kilichomfanya huyo mtu amwone Yesu na kupiga kelele ni ule upako uliokuwa ndani ya Yesu. Huo upako ndiyo Roho Mtakatifu.

Unaweza ukawa na Roho Mtakatifu lakini usiwe na nguvu za Roho Mtakatifu. Mtu anapoamini na kubatizwa anampokea Roho Mtakatifu lakini nguvu za Roho Mtakatifu ni kibarua kingine.

Ukipokea nguvu ya Roho Mtakatifu unapokea mamlaka, amri, na uweza wa kuvunja na kuharibu na kuangamiza madhabahu ya ufalme wa giza.

Nguvu ya Roho Mtakatifu inakuja kwa kufunga na kuomba na kusoma neno kwa wingi

Matayo 17:21; “[Lakini namna hii haitoki ila kwa kusali na kufunga.]”

Mtu aliye na nguvu za Roho Mtakatifu;

  1. Anasimama imara kwenye maombi.
  2. Anafunga na kuomba,
  3. Anasoma neno mara kwa mara’
  4. Hachelewi ibadani’
  5. Anasifu na kuabudu

“Katika siku ya mwisho, siku ile kubwa ya sikukuu, Yesu akasimama, akapaza sauti yake akisema, Mtu akiona kiu, na aje kwangu anywe. Aniaminiye mimi, kama vile maandiko yalivyonena, mito ya maji yaliyo hai itatoka ndani yake. Na neno hilo alilisema kuhusu Roho, ambaye wale wamwaminio watampokea baadaye; kwa maana Roho alikuwa hajaja, kwa sababu Yesu alikuwa hajatukuzwa.” Yohana 7:37-39 SUV

Roho Mtakatifu anaviwango (vipimo)

Kuna viwango vya kumpokea Roho Mtakatifu ili atende makuu kwako.

“Yesu akajibu, akamwambia, Kila anywaye maji haya ataona kiu tena; lakini yeyote atakayekunywa maji yale nitakayompa mimi hataona kiu milele; bali yale maji nitakayompa yatakuwa ndani yake chemchemi ya maji, yakibubujikia uzima wa milele.” Yohana 4:13-14 SUV

Unamchukuliaje Yesu maishani mwako? Ukimchukulia Yesu viwango vya chini na Roho Mtakatifu atakaa kwako viwango vya chini na utakuwa wa kukimbilia kuombewa tu huku silaha ya injili unayo.

Ndani ya Roho Mtakatifu kuna uzima wa milele.

“Basi atukuzwe yeye awezaye kufanya mambo ya ajabu mno kuliko yote tuyaombayo au tuyawazayo, kwa kadiri ya nguvu itendayo kazi ndani yetu;” Waefeso 3:20 SUV

Hiyo nguvu inayotenda kazi ndani yako ni nguvu ya ROHO Mtakatifu

“Kwa kuwa yeye aliyetumwa na Mungu huyanena maneno ya Mungu; kwa sababu hamtoi Roho kwa kipimo.” Yohana 3:34 SUV

Mungu wetu anataka tunene ya kwake kwa msaada wa Roho Mtakatifu. Roho Mtakatifu anakuonyesha namna ya kutenda

“Basi nasema, Nendeni kwa Roho, wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili. Kwa sababu mwili hutamani ukishindana na Roho, na Roho kushindana na mwili; kwa maana hizi zimepingana, hata hamwezi kufanya mnayotaka.” Wagalatia 5:16-17 SUV

Ukiwa na Roho Mtakatifu unakuwa na moto wa Mungu

“Kweli mimi nawabatiza kwa maji kwa ajili ya toba; bali yeye ajaye nyuma yangu ana nguvu kuliko mimi, wala sistahili hata kuvichukua viatu vyake; yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu na kwa moto.” Mathayo 3:11 SUV

“Wakati ilipotimia siku ya Pentekoste walikuwako wote mahali pamoja. Kukaja ghafla toka mbinguni sauti kama mvumo wa upepo mkali ukienda kasi, ukaijaza nyumba yote waliyokuwa wameketi. Kukawatokea ndimi zilizogawanyikana, kama ndimi za moto uliowakalia kila mmoja wao. Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia kutamka.” Matendo 2:1-4 SUV

Moto unaozungumziwa hapa ni ROHO Mtakatifu.

“Na katika kile kiti cha enzi kunatoka umeme na sauti na ngurumo. Na taa saba za moto zikiwaka mbele ya kile kiti cha enzi, ndizo Roho saba za Mungu.” Ufunuo 4:5 SUV

Zile taa saba ni roho saba za Mungu (Isaya 11:2-3)

  1. Roho ya Uchaji;
  2. Roho ya maarifa;
  3. Roho ya Ushauri;
  4. Roho ya uweza;
  5. Roho ya Bwana;
  6. Roho ya Ufahamu;
  7. Roho ya hekima

Roho Mtakatifu anakufanya waovu wakukimbie kwa kuwa wewe ni mwali wa moto. Hakuna awezaye kukusogelea.

“Na kuhusu malaika asema, Awafanya malaika wake kuwa pepo, Na watumishi wake kuwa miali ya moto.” Waraka kwa Waebrania 1:7 SUV

“Kwa maana mimi, asema BWANA, nitakuwa ukuta wa moto kuuzunguka pande zote, nami nitakuwa huo utukufu ndani yake.” Zekaria 2:5 SUV

Neno la Mungu ni Roho.

Bwana akujaze Roho Mtakatifu ukawe ukuta wa moto waovu wakikuona wakuite mtumishi wa Mungu hata kabla hujawaambia.

“Kwa sababu hiyo BWANA, Mungu wa majeshi, asema hivi, Kwa sababu mnasema neno hili, tazama, nitafanya maneno yangu katika kinywa chako kuwa moto, na watu hawa kuwa kuni, nao moto utawala.” Yeremia 5:14 SUV

“Wenye dhambi walio katika Sayuni wanaogopa; tetemeko limewashika wasiomcha Mungu; Ni nani kwetu sisi awezaye kukaa na moto uangamizao; ni nani kwetu sisi awezaye kukaa na moto uteketezao milele?” Isaya 33:14 SUV

“maana Mungu wetu ni moto ulao.” Waraka kwa Waebrania 12:29 SUV

Ndivyo ilivyo waovu humkimbia mtu mwombaji.

Karama na vipawa mtu hupewa na Roho Mtakatifu;

“Basi kuna karama tofauti; bali Roho ni yeye yule. Tena kuna huduma tofauti, na Bwana ni yeye yule. Kisha kuna uwezo tofauti wa kutenda kazi, bali Mungu ni yeye yule azitendaye kazi zote katika wote. Lakini kila mmoja hupewa ufunuo wa Roho kwa kufaidiana. Maana mtu mmoja kwa Roho apewa neno la hekima; na mwingine neno la maarifa, apendavyo Roho yeye yule; mwingine imani katika Roho yeye yule; na mwingine karama za kuponya katika Roho yule mmoja;” 1 Wakorintho 12:4-9 SUV

Karama ya uponyaji, miujiza, kupambanua roho, na aina za lugha. Hii ni kazi ya Roho Mtakatifu

Huduma mtu hupewa na Roho Mtakatifu;

“Na Mungu ameweka wengine katika kanisa, wa kwanza mitume, wa pili manabii, wa tatu waalimu, kisha miujiza, kisha karama za kuponya wagonjwa, aina za usaidizi, maongozi na aina za lugha.” 1 Wakorintho 12:28 SUV

Kuna huduma ya Uinjilist, Utume, Unabii, Ualimu, Uchungaji, na Ushemasi. Huduma hizi mtu hupewa na Roho Mtakatifu

Je, Roho Mtakatifu anaweza kukimbia?

Ndiyo anaweza kukukimbia na ukabaki kama gari lisilo na mafuta.

“Msimzimishe Roho;” 1 Wathesalonike 5:19 SUV

Mambo matatu yanaweza kumfanya Roho Mtakatifu akimbie kwa mtu;

  • Kutenda dhambi.
  • Kutokutii
  • Kumkataa Yesu na kazi zake zote

“Naye akiisha kusema hayo, akawavuvia, akawaambia, Pokeeni Roho Mtakatifu.” Yohana 20:22 SUV

Maana ya kuzimisha ni kukifanya kitu kisionekane tena kama moto unauzima kwa maji na ukazima ndivyo ilivyo na Mtakatifu mtu humzima kwa dhambi, kutotii na kumkataa Yesu.

Sifa ya kwanza ya kumpokea Roho Mtakatifu ni kumkubali Yesu, mtu asimpomkubali Yesu hawezi kumpokea Roho Mtakatifu

MUNGU AWABARIKI SANA

Naitwa Peter Francis, Nipo Mtwara Tanzania.

Nawapenda sana