ROHO MTAKATIFU DAY ONE:

Ninayewasilisha naitwa Mwl. Gambo Jnr. Gambo

https://biblianijibulako.wordpress.com

⭐biblia ni jibu lako⭐ 20180126_095329619662689..jpg

UTANGULIZI:

Roho mtakatifu ni Roho ya/wa Mungu, ni Mungu mwenyewe, ni nafsi moja kati ya tatu za Mungu. Roho mtakatifu ni msaidizi wetu, ni ahadi ya Kristo kwetu sisi. Mara pengine anatambulishwa katika agano la kale kama Roho ya Bwana. Roho mtakatifu ana sifa nyingi, ambazo ni pamoja na kwamba ni roho, ni mtakatifu sana, haonekani kwa macho ya nyama ila ya rohoni na anaonekana kama hua/njiwa, moto, maji, upepo nk.

KAZI ZA ROHO MATAKATIFU KWETU SISI:-

  1. Ni msaidizi wetu. Anatusaidia katika udhaifu wetu. 

“Lakini mimi nawaambia iliyo kweli; yawafaa ninyi mimi niondoke, kwa maana mimi nisipoondoka, huyo Msaidizi hatakuja kwenu; bali mimi nikienda zangu, nitampeleka kwenu.” Yohana 16:7

  1. Anauhakikisha ulimwengu kwa habari ya dhambi, haki na hukumu. 

“Naye akiisha kuja, huyo atauhakikisha ulimwengu kwa habari ya dhambi, na haki, na hukumu. Kwa habari ya dhambi, kwa sababu hawaniamini mimi; kwa habari ya haki, kwa sababu mimi naenda zangu kwa Baba, wala hamnioni tena; kwa habari ya hukumu, kwa sababu yule mkuu wa ulimwengu huu amekwisha kuhukumiwa.” Yohana 16:8-11

  1. Ni kiongozi. Anatuongoza katika kweli yote. 

“Lakini yeye atakapokuja, huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote; kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena, na mambo yajayo atawapasha habari yake. Yeye atanitukuza mimi, kwa kuwa atatwaa katika yaliyo yangu na kuwapasha habari. Na yote aliyo nayo Baba ni yangu; kwa hiyo nalisema ya kwamba atatwaa katika yaliyo yangu, na kuwapasheni habari.” Yohana 16:13-15

  1. Ni mwombezi wetu. Anatuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkika. 

“Kadhalika Roho naye hutusaidia udhaifu wetu, kwa maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo, lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa. Na yeye aichunguzaye mioyo aijua nia ya Roho ilivyo, kwa kuwa huwaombea watakatifu kama apendavyo Mungu.” Warumi 8:26-27

  1. Ni shuhuda wa injili ya Yesu Kristo. 

“Lakini ajapo huyo Msaidizi, nitakayewapelekea kutoka kwa Baba, huyo Roho wa kweli atokaye kwa Baba, yeye atanishuhudia. Nanyi pia mnashuhudia, kwa kuwa tangu mwanzo mmekuwapo pamoja nami.” Yohana 15:26-27

  1. Ni mlinzi wetu. Anatulinda hata tutakapoufikilia ule mwisho. 

“Ahimidiwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kwa rehema zake nyingi alituzaa mara ya pili ili tupate tumaini lenye uzima kwa kufufuka kwake Yesu Kristo katika wafu; tupate na urithi usioharibika, usio na uchafu, usionyauka, uliotunzwa mbinguni kwa ajili yenu. Nanyi mnalindwa na nguvu za Mungu kwa njia ya imani hata mpate wokovu ulio tayari kufunuliwa wakati wa mwisho.” 1 Petro 1:3-5

ROHO MTAKATIFU TANGU MWANZO:

Maandiko yanamtaja Roho matakatifu akijidhihirisha na kwamba kwake kazi kubwa na miujiza yenye nguvu imekuwa ikitendeka. Tunaiona nguvu za Roho matakatifu tangu uumbaji, na kwake uumbaji wote ukafanyika. 

“Hapo mwanzo Mungu aliziumba mbingu na nchi. Nayo nchi ilikuwa ukiwa, tena utupu, na giza lilikuwa juu ya uso wa vilindi vya maji; Roho ya Mungu ikatulia juu ya uso wa maji.” Mwanzo 1:1-2

Pia tunaona katika kipindi cha Agano la kale, Roho Mtakatifu aliwashukia watu fulani fulani ili kutimiza matakwa na mapenzi ya Mungu.

Bazaleli alijazwa Roho Mtakatifu ili kuitimiza kazi ya Mungu ya ufundi stadi.

“Angalia, nimemwita kwa jina lake Bezaleli mwana wa Uri, mwana wa Huri, wa kabila ya Yuda; nami nimemjaza roho ya Mungu, katika hekima, na maarifa, na ujuzi, na mambo ya kazi ya kila aina, ili abuni kazi za ustadi, kuwa fundi wa dhahabu, na wa fedha, na wa shaba, na kukata vito kwa kutiwa mahali, na kuchora miti, na kufanya kazi ya ustadi iwayo yote.” Kutoka 31:2-5

Roho Mtakatifu alimjaa Yoshua mwana wa Nuni ili kuwaongoza wana wa Mungu, Taifa la Israel.

“Musa akanena na Bwana akisema, Bwana, Mungu wa roho za wenye mwili wote, na aweke mtu juu ya mkutano, atakayetoka mbele yao, na kuingia mbele yao; atakayewaongoza watokapo, na kuwaleta ndani; ili mkutano wa Bwana wasiwe kama kondoo wasio na mchungaji. Bwana akamwambia Musa, Mtwae Yoshua, mwana wa Nuni, mtu mwenye roho ndani yake, ukamwekee mkono wako;” Hesabu 27:15-18

Lakini pia tunaona Roho Mtakatifu alimshukia Daudi ili asimame kama Mfalme katika nafasi ya mfalme Sauli.

“Ndipo Samweli akaitwaa pembe yenye mafuta, akamtia mafuta kati ya ndugu zake; na roho ya Bwana ikamjilia Daudi kwa nguvu tangu siku ile. Basi Samweli akaondoka, akaenda zake Rama.” 1 Samweli 16:13

Pamoja na hayo, Roho Mtakatifu hakuishi na wanadamu katika kipindi cha Agano la kale, bali alikuwa anashukuka wakati wa kufanya kazi maalum ambayo kimsingi huyo mtumishi wake Mungu asingeweza mwenyewe bila msaada (Roho Mtakatifu ni msaidizi).

Tunajifunza hili kwa Samson ambaye alikuwa na nguvu sana. Lakini pamoja na nguvu zake, kila alipokuwa akifanya jambo fulani, alishukiwa na nguvu za ziada ambazo ni za Roho matakatifu. 

“Ndipo Samsoni na baba yake na mama yake wakatelemkia Timna, wakafika mashamba ya mizabibu huko Timna; na tazama, mwana-simba akamngurumia. Roho ya Bwana ikamjilia kwa nguvu, naye akampasua kana kwamba anampasua mwana-mbuzi, wala hakuwa na kitu cho chote mkononi mwake; lakini hakuwaambia baba yake na mama yake aliyoyafanya.” Waamuzi 14:5-6.

Roho ya Bwana ikamjilia juu yake kwa nguvu, naye akatelemkia Ashkeloni, akapiga watu waume thelathini katika watu hao, na kuzitwaa nyara zao, na kuwapa hao waliokitambua kitendawili mavao hayo. Hasira zake zikamwaka, naye akakwea kwenda nyumbani kwa baba yake.” Waamuzi 14:19.

“Alipofika Lehi, Wafilisti wakapiga kelele walipokutana naye; ndipo roho ya Bwana ikamjia kwa nguvu, na zile kamba zilizokuwa juu ya mikono yake zikawa kama kitani iliyoteketezwa kwa moto, na vile vifungo vyake vikaanguka mikononi mwake. Naye akaona mfupa mbichi wa taya ya punda, akautwaa, akapiga watu elfu kwa mfupa huo;” Waamuzi 15:14-15

Hivyo ndivyo alivyofanya kazi Roho Mtakatifu katika kipindi chote cha Agano la kale.

ROHO MATAKATIFU KATIKA KIPINDI CHA AGANO JIPYA:

Wakati wa maisha yake kimwili duniani, Yesu Kristo alijazwa kwa uwezo wa Roho Mtakatifu (Luka 4:1), ndipo akaongozwa na Roho Mtakatifu (Luka 4:14) akajazwa nguvu na Roho Mtakatifu (Matt. 28:20).

Na hata kabla hajapaa, Yesu Kristo alituahidi sisi wanafunzi wake kwamba tutampokea msaidizi ambaye ni Roho Mtakatifu; aje akae pamoja nasi tusiwe wapweke. 

“Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele; ndiye Roho wa kweli; ambaye ulimwengu hauwezi kumpokea, kwa kuwa haumwoni wala haumtambui; bali ninyi mnamtambua, maana anakaa kwenu, naye atakuwa ndani yenu. Sitawaacha ninyi yatima; naja kwenu.” Yohana 14:16-18

“Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi.” Matendo ya Mitume 1:8

Hata ilipotimia ile siku ya Pentekoste, hakika Roho Mtakatifu alishuka kwa nguvu ya ajabu. Wanafunzi walikuwa pamoja wakazwa nguvu katika Roho Mtakatifu, kila mmoja akaotwa na ndimi za kununa kwa lugha nyingine. Ni Yesu Kristo alitimiza ahadi yake, na sasa Roho matakatifu atakaa pamoja nasi tukiwa katika utakatifu ndani ya wokovu. 

“Hata ilipotimia siku ya Pentekoste walikuwako wote mahali pamoja. Kukaja ghafula toka mbinguni uvumi kama uvumi wa upepo wa nguvu ukienda kasi, ukaijaza nyumba yote waliyokuwa wameketi. Kukawatokea ndimi zilizogawanyikana, kama ndimi za moto uliowakalia kila mmoja wao. Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia kutamka.” Matendo ya Mitume 2:1-4

Ahadi ya Yesu hapo sasa inatimia, yeye amepaa lakini Roho Mtakatifu ameshuka kuweka makao nasi.

Kwahiyo tunaona tofauti katika kudhihirika kwa Roho Mtakatifu kipindi cha Agano la kale na kipindi cha Agano jipya ni hii… Agano la Kale hajaweka makao, alikuwa anashuka tu na kuondoka lakini kipindi cha Agano Jipya amekuja kuweka makao pamoja nasi.

KUJAZWA ROHO MTAKATIFU NA KUJAZWA NA ROHO MTAKATIFU:

Hapa tunaona mambo makuu mawili ambayo mara nyingi wapendwa wengi wamekuwa wanayachukulia kitu kimoja. Mambo hayo ni;

  1. Kujazwa Roho Mtakatifu na
  2. Kujazwa na Roho Mtakatifu

KUJAZWA ROHO MTAKATIFU:

“Tena msilewe kwa mvinyo, ambamo mna ufisadi; bali mjazwe Roho;” Waefeso 5:18

Kwanza kabisa kwa hili swala la kujazwa ROHO Mtakatifu, turejee kwenye ahadi ya Yesu Kristo. Yesu aliahidi kwamba atashuka akae pamoja nasi yeye atakapopaa.

Maana yake ni kwamba Roho mtakatifu sasa yupo kikazi ulimwenguni, lakini walimwengu hawamwoni kwasababu mbili;

  • Hawaoni rohoni na
  • Hawamjui Roho mtakatifu.

Tunapomwamini Bwana Yesu Kristo maana yake tunaamini pia Neno lake. Roho mtakatifu anakaa pamoja nasi tena anakaa milele. 

“Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele;” Yohana 14:16

Kumbe basi, tunapookoka (tunapoamini na kukiri kwamba Yesu ndiye Kristo) tunakuwa tumeingia katika uwepo Roho mtakatifu na siyo kujazwa Roho mtakatifu. Tunakuwa tunamwamini Roho mtakatifu na kazi zake.

“Aniaminiye mimi, kama vile maandiko yalivyonena, mito ya maji yaliyo hai itatoka ndani yake. Na neno hilo alilisema katika habari ya Roho, ambaye wale wamwaminio watampokea baadaye; kwa maana Roho alikuwa hajaja, kwa sababu Yesu alikuwa hajatukuzwa.” Yohana 7:38-39

Roho alikuwa hajaja… Kwasababu Yesu alikuwa hajatukuzwa

Nanyi pia katika huyo mmekwisha kulisikia neno la kweli, habari njema za wokovu wenu; tena mmekwisha kumwamini yeye, na kutiwa muhuri na Roho yule wa ahadi aliye Mtakatifu.” Waefeso 1:13

Mmekwisha kumwamini na kutiwa muhuri na Roho Mtakatifu

Kwasababu unakuwepo katika uwepo wa Roho mtakatifu, maana yake upo katika sehemu ambayo unaweza kujazwa Roho mtakatifu. Kama utavikwepa vizuizi vyote ambavyo vinakufanya usijazwe roho mtakatifu, hakika yako unajazwa.

Vizuizi hivyo ni pamoja na dhambi, kutokuokoka, kutokutii, kutokuwa tayari na kutokuwa na neno la Mungu ndani yako. Roho Mtakatifu anapoweka makao ndani yako maana yake ufalme wa Mungu wote upo ndani yako (1 Yoh. 3:24)

Ukiviepuka na kuvishinda vizuizi hivyo, unapaswa kutulia katika maombi, unayafanya maombi ya kuzungumza na Mungu; unaomba na unamsikiliza, hoja yako kubwa ni utakatifu na usafi wa nafsi ili ombi lako la kujazwa Roho mtakatifu litimie sasa.

Baada ya hapo Roho mtakatifu anakaa ndani yako sasa, siyo tu anaishi pamoja nasi bali yupo ndani yetu tuliojazwa

Ila Roho mtakatifu anaweza kufurahishwa au kuhuzunishwa (Efe. 4:30). Kama amehuzunika na kazi yake ndani yetu inapoa/inazimia (1Thes.5:19).

“Wala msimhuzunishe yule Roho Mtakatifu wa Mungu; ambaye kwa yeye mlitiwa muhuri hata siku ya ukombozi.” Waefeso 4:30.

“Msimzimishe Roho;” 1 Wathesalonike 5:19

Sasa ili kudumu na Roho mtakatifu ndani mwetu, kumtunza akae na azae humo tunapaswa kudumu katika maombi, katika neno la Mungu, katika utumishi kwa Mungu na katika ushirika.

KUJAZWA NA ROHO MTAKATIFU:

Roho mtakatifu akikaa ndani yetu, yaani tukijaa/tukijazwa Roho mtakatifu na yeye anatujaza mambo mazuri sana katika kuujenga mwili Kristo kwa kutunza umoja wa kanisa.

Mambo hayo ni;

  1. Tunda la Roho (Gal.5:22)

“Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sharia.” Wagalatia 5:22-23

Ukijazwa Roho Mtakatifu, utajitambua kwa kuona kama ndani yako kuna tunda la Roho… Kama hauna tunda lake maana yake hauna au haujajazwa Roho Mtakatifu.

  1. Karama (vitendea kazi vya kiroho) (1Kor. 12:3-11)

“Basi kuna aina mbalimbali za karama, lakini Roho ni yule yule. Pia kuna huduma za aina mbalimbali, lakini Bwana ni yule yule. Kisha kuna tofauti za kutenda kazi, lakini ni Mungu yule yule atendaye kazi zote kwa watu wote.   Basi kila mmoja hupewa ufunuo wa Roho kwa faida ya wote. Maana mtu mmoja kwa Roho hupewa neno la hekima na mwingine neno la maarifa kwa Roho huyo huyo. Mtu mwingine imani kwa huyo Roho na mwingine karama za kuponya. Kwa mwingine matendo ya miujiza, kwa mwingine unabii kwa mwingine kupambanua roho, kwa mwingine aina mbalimbali za lugha, kwa mwingine tafsiri za lugha. Haya yote hufanywa na huyo huyo Roho mmoja, Roho naye humgawia kila mtu, kama apendavyo mwenyewe.   Kama vile mwili ulivyo mmoja nao una viungo vingi, navyo viungo vyote vya mwili ingawa ni vingi, ni mwili mmoja, vivyo hivyo na Kristo.” 1 Wakorintho 12:4-12 NEN

Katika maandiko haya tunapa makundi matatu ya karama tisa za Roho Mtakatifu;

  1. Kundi la kwanza; karama za ufunuo ambzo ni Neno la hekima, kupambanua Roho na Neno la maarifa.
  2. Kundi la pili; karama za uwezo na nguvu ambazo ni Imani, kuponya na matendo ya miujiza.
  3. Kundi la tatu; karama za usemi ambazo ni unabii, aina za lugha na kufasiri lugha.

Roho Mtakatifu anatujaza karama ambayo inakufaa kama kitendea Kazi cha kiroho. Hizi karama sasa ndipo zinakuja kunisaidia katika Kazi za kiroho, HUDUMA

  • Huduma (Kazi za kiroho)

“Naye alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu; kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe;” Waefeso 4:11-12

Katika maandiko tunapata huduma kuu tano za Roho Mtakatifu;

  1. Mitume
  2. Manabii
  3. Wainjilisti
  4. Wachungaji
  5. Waalimu

Sasa huduma hizi hatimaye zinakuja kukamilisha Kazi za ujenzi wa kanisa la Mungu ambalo ndiyo mwili wa Kristo.

Mungu awabariki sana san asana.