DHANA YA KWANZA;

MAOMBI ni mazungumzo huru kati ya mtu au kundi la watu na Mungu.

Mazungumzo maana yake ni kitendo cha kusemezana na kusikilizana. Yaani mmoja anazungumza mwingine anasikiliza na kusikia, hatimaye msikilizaje anajibu na mzungumzaji anasikiliza ili asikie.

Katika kitabu cha Isaya 1:18, maandiko yanasema; “Haya, njooni, tusemezane, asema Bwana; …” yaani Mungu anatoa nafasi kwetu sisi tutakaokuwa tayari, kusema naye!

Maana ya kusemezana na Mungu kwetu sisi ndiyo kuomba, tunaita maombi.

Maandiko yanasema tena katika kitabu cha nabii Isaya 43:26 kwamba; “Unikumbushe, na tuhojiane; eleza mambo yako, upate kupewa haki yako.” …yaani Mungu anaendelea kutuambia sisi kwamba tumkumbushe, tena TUHOJIANE naye, kwa maana ya kuzungumza naye.

Anasema eleza mambo yako, upate kupewa haki yako yaani usipoeleza mambo yako, ambayo ndiyo haki yako; Mungu hawezi kukupa haki yako.

Namna ya kupata haki yako ni kuzungumza na Mungu. Kuzungumza na Mungu ni kuomba.

Aina ya mazungumzo yetu na Mungu ni KUHOJIANI yaani kila upande unakuwa na sifa ya;

1) Kuongea kinachoeleweka,
2) Kusikiliza ili kusikia.

Mungu wetu anasikia; anayo hiyo sifa ya kusikia hivyo tunapoomba, yaani tunaposema naye; Yeye anatusikia na anatujibu.

Biblia inasema katika Isaya 59:1; “… sikio lake si zito, hata lisiweze kusikia” maandiko yanasema kwa habari ya Mungu, kwamba sikio lake si zito lisiweze kusikia.

Katika Yeremia 8:6 maandiko yanasema; “Nalisikiliza nikasikia, lakini walisema yasiyo sawa; hapana mtu aliyetubia maovu yake, akisema, Nimefanya nini? Kila mtu hurudia mwendo wake mwenyewe, kama farasi aendavyo kasi vitani.”

Kumbe tunapoomba, Mungu anasikiliza na tena anasikia.

Kusikiliza ni kazi ya masikio, kusikia ni kazi ya moyo.

Kusikia ni sawa sawa na kutii. Kutii maana yake ni kupokea ujumbe na kuufanyia kazi.

Mtu aliyesikia maana yake anajibu NDIYO NITAFANYA na anafanya kweli, au anasema HAPANA SIFANYI na hafanyi kweli.

Soma Kutoka mlango wa 3 utaona mahojiano baina ya Mungu na Musa.

Kutoka 3:4 inasema; “Bwana alipoona ya kuwa amegeuka ili atazame, Mungu akamwita kutoka katikati ya kile kijiti, akasema, Musa! Musa! Akasema, Mimi hapa.”

Mungu anamwita Musa na Musa anaitika; baada ya hapo ni mahojiano baina ya Mungu na Musa.

Ona hili andiko tena; katika II Nyakati 7:14 Biblia inasema; “ikiwa watu wangu, walioitwa kwa jina langu, watajinyenyekesha, na kuomba, na kunitafuta uso, na kuziacha njia zao mbaya; basi, nitasikia toka mbinguni, na kuwasamehe dhambi yao, na kuiponya nchi yao.”

…ninachukua ujumbe huu na kuugawa katika mafungu makuu matatu; kwanza, watu wa Mungu kuomba lakini pili, Mungu kusikia na hatimaye tatu, Mungu kujibu maombi ya watu wake.

PATA MWENDELEZO, BOFYA HAPA DHANA YA PILI