Na; Magdalena Felician, A/C BJL.

Andiko la kusimamia; ❝Msimzimishe Roho;❞

—1 Wathesalonike 5: 19 (Biblia Takatifu)


YALIYOMO:

  1. Madhabahu ni nini?
  2. Moto wa madhabahu ni nini?
  3. Njia zipi zitumike kuutunza moto wa madhabahu?
  4. Mengineyo.

UTANGULIZI:

Madhabahu ni eneo lililotengwa na kuwekwa wakfu kwa ajili ya kufanyia IBADA.

Ibada ni kitendo cha kumuabudu, kumtukuza na kutoa dhabihu za shukurani mbele za Mungu/ miungu.

Kuna aina kuu mbili za madhabahu:-

  • Madhabahu ya Mungu aliye hai (YEHOVA).
  • Madhabahu za kishetani.

Madhabahu inakamilishwa na vitu vikuu vitatu:-

1) Mungu wa madhabahu.
2) Kuhani wa madhabahu.
3) Sadaka

Chimbuko lolote la Ibada linaanzia madhabahuni. Kwani ndani ya madhabahu ndipo mahali pekee ambapo Mungu wa madhabahu huteremka na kuketi.

NAMNA YA KUTUNZA MOTO WA MADHABAHU ILI USIZIMIKE.

Maswali la kutafakari kipindi tunaendelea mbele.

  • Moto huo ni nini.?
  • Kwanini tuutunze moto wa madhabahu ili usizimike?
  • Je, moto huo una faida gani kwetu sisi?

Chimbuko la somo letu linatokea katika agizo hili alilopewa Musa, aende akamwambie Haruni ambaye kwa kipindi hicho ndiye aliyekuwa kuhani wa hekalu la Bwana.

Haya, mwagize Haruni na wanawe, uwaambie, Amri ya sadaka ya kuteketezwa ni hii; hiyo sadaka ya kuteketezwa itakuwa pale motoni juu ya madhabahu usiku wote hata asubuhi; na huo moto wa madhabahu utawaka juu yake usizimike… Na huo moto ulio madhabahuni atautunza uwake daima juu yake, usizimike; naye kuhani atateketeza kuni katika moto huo kila siku asubuhi; naye ataipanga sadaka ya kuteketezwa juu yake, naye atayateketeza mafuta ya sadaka za amani juu yake.
Moto utatunzwa uwake juu ya madhabahu daima; usizimike.
—Mambo ya Walawi 6: 9, 12-13 (Biblia Takatifu)

Moto huo ambao Haruni anaagizwa kuuchochoea kila siku asubuhi na usiku ili usizimike, kwa mara ya kwanza kabisa baada ya kujengwa madhabahu moto ulishuka kutoka juu mbinguni.

Kazi kuu ya huo moto ilikuwa ni kwa ajili ya kuteketeza sadaka mbalimbali zilizokuwa zinaletwa na watu kwa ajili ya UPATANISHO yani ondoleo la dhambi zao (utakaso).

Mambo yote yaliyofanyika ktk kipindi kile cha torati, yalikuwa ni kivuli cha haya yajayo.

Basi torati, kwa kuwa ni kivuli cha mema yatakayokuwa, wala si sura yenyewe ya mambo hayo, kwa dhabihu zile zile wanazozitoa kila mwaka daima, haiwezi wakati wo wote kuwakamilisha wakaribiao.
—Waebrania 10: 1 (Biblia Takatifu)

Agizo hilo la kuutunza moto wa madhabahu kwetu sisi leo limekuwa ni jambo la rohoni, kwani sisi tuliokombolewa kwa damu ya Yesu hatuenendi tena ktk mwili bali twaenenda ktk Roho.

KIINI CHA SOMO LETU

Madhabahu halisi inayozungumziwa hapo ni MOYO WA MWANADAMU. Moyo ndiyo main engine ya maisha ya mwanadamu. Moyoni ndipo sehemu maalum panapo hifadhiwa nyaraka na rasilimali mbalimbali kwa ajili ya manufaa ya maisha yetu. Moyo ndio usukani wa maisha yetu, pia moyo ndio MAKAO MAKUU YA MUNGU.

Kwanini moyoni ndiyo sehemu pekee ambapo Mungu alipachagua kuweka makao yake?…Kwasababu MOYO ndio sehemu pekee iliyobeba HATIMA YA MAISHA YA MTU.

Ndani ya moyo ndipo palipo na MATAKWA YA JAMBO LOLOTE; Chimbuko la uzima wa mtu linaanzia moyoni. Chimbuko la uovu, tamaa, kiburi, dharau, majivuno na uasi vyote hivyo vinaanzia ndani ya moyo.

Ukitaka kuamini haya ninayosema soma haya maandiko hapa chini.

Linda moyo wako kuliko yote uyalindayo; Maana ndiko zitokako chemchemi za uzima.
—Mithali 4: 23 (Biblia Takatifu)

Moyo ndio umebeba uzima wa mtu, ila moyo huohuo unaouwezo wa kukusababishia mauti.

Moyo huwa mdanganyifu kuliko vitu vyote, una ugonjwa wa kufisha; nani awezaye kuujua?
—Yeremia 17: 9 (Biblia Takatifu)

Hapo, Bibilia inaposema moyo una ugonjwa wa kufisha ni nani awezaye kuujua? …ina maana kwamba, moyo una ugonjwa wa kuua, yani kusababisha mauti na aujuaye huo ugonjwa kuutibu ni Mungu pekee.

Kwahiyo tiba pekee ya huo ugonjwa wa moyo ni Mungu pekee. Ndio maana Mungu amechagua makazi yake yawe ndani ya moyo ili au-control ipasavyo usije kukusababishia mauti ya milele.

Tuendelee na somo letu, namna ya kuutunza moto wa madhabahu ili usizimike.

Tumeshaona hapo juu kwamba madhabahu inayozungumziwa hapo ni MOYO. Moto wenyewe ni ishara ya ROHO MTAKATIFU yani ni MUNGU MWENYEWE.

maana Mungu wetu ni moto ulao.
—Waebrania 12: 29 (Biblia Takatifu)

Ile siku ulipoamini moyoni mwako kuwa Yesu ni Bwana na mkombozi wa maisha yako, ukaamua kuacha mambo yote na ukamruhusu Mungu aingie moyoni mwako. Hiyo ndiyo siku ambayo, Moto wa Mungu ulishuka kutoka juu ukaingia moyoni mwako.

Mimi na wewe tu makuhani wa Yesu. Maana ya kuhani ni mjumbe wa Mungu.

Kwa maana yapasa midomo ya kuhani ihifadhi maarifa, tena yawapasa watu kuitafuta sheria kinywani mwake; kwa kuwa yeye ni mjumbe wa Bwana wa majeshi.
—Malaki 2: 7 (Biblia Takatifu)

Kama Haruni alivyopewa agizo la kuuchochoea moto wa madhabahu ili usizimike mchana na usiku, jukumu hilo imetupasa kuliendeleza sisi leo hii ambao tu makuhani wa Mungu aliye hai. Mioyo yetu ndio madhabahu ya kuutunza moto ili usizimike. Ila, tambua kwamba usipofanya bidii na juhudi ya kuuchochoea mchana na usiku, ni lazima moto uzimike. Na faida ya huo moto ni kwamba:-

  1. Unaleta upatanisho au ushirika baina yetu sisi na Mungu.
  2. Unatekeza kila aina ya uchafu.
  3. Unasafisha na kutakasa mioyo yetu.
  4. Unatupa uzima wa milele.
  5. Kazi ya moto ni kung’arisha dhahabu. Hivyo, mimi na wewe tu dhahabu mbele za Mungu. Tunapopitia ktk magumu, kazi ya moto ni kutuimarisha na kutufanya tung’are muda wote

Msimzimishe Roho;
—1 Wathesalonike 5: 19 (Biblia Takatifu)

Usiruhusu kumzimisha Roho wa Mungu ndani yako. Yeye ni mfano wa TUNU YA THAMANI katika maisha yetu.

Yupo tayari kukupa leo tumaini la maisha yako yajayo endapo tu utamruhusu aendeshe maisha yako. Tazama anavyosema.

Mwanangu, nipe moyo wako; Macho yako yapendezwe na njia zangu.
—Mithali 23: 26 (Biblia Takatifu)

Jukumu la kumpa moyo wako wote lipo mikononi mwako, usiruhusu moyo wako ukuhadae kwa tamaa za hapa duniani.

MAMBO YA KUFANYA ILI KUUTUNZA MOTO UZIMIKE JUU YA MADHABAHU:

1. Kufanya toba na kuungama kila wakati (UTAKASO)

Mungu wetu ni Mtakatifu, nasi pia imetupasa kuwa watakatifu. Ila, kwakuwa asili ya mwanadamu tangu awali ni uovu basi tusiache kuungama dhambi zetu kila iitwapo leo.

Afichaye dhambi zake hatafanikiwa; Bali yeye aziungamaye na kuziacha atapata rehema.
—Mithali 28: 13 (Biblia Takatifu)

2. Kusoma Neno la Mungu.

Neno la Mungu ni chakula cha uzima, Neno la Mungu ni taa yetu tena ni ngao yetu. Ndani ya Neno ndipo ambapo tunapata uzima na amani mioyoni mwetu. Neno linatuongoza katika njia sahihi.

Moyoni mwangu nimeliweka neno lako, Nisije nikakutenda dhambi.
—Zaburi 119: 11 (Biblia Takatifu)

3. Kufunga na kuomba kwa bidii.

Tunakaa ktk dunia iliyojaa dhiki za kila aina, imetupasa kumuomba Mungu siku zote pasipo kukata tamaa. Tumtafute Mungu kwa bidii kwa njia ya kufunga na kuomba ili atuwezeshe kumaliza safari yetu salama.

ombeni bila kukoma;
—1 Wathesalonike 5: 17 (Biblia Takatifu)

Ukizingatia hayo mambo matatu, utafananishwa na wale wanawali watano wenye hekima. Lakini, usipoyafanya hayo mambo matatu, utafananishwa na wale wanawali watano wapumbavu ambao walikutwa na Bwana arusi taa zao zimezika.

Mathayo 25:6-13 (Biblia Takatifu)
⁶ Lakini usiku wa manane, pakawa na kelele, Haya, bwana arusi; tokeni mwende kumlaki.
⁷ Mara wakaondoka wanawali wale wote, wakazitengeneza taa zao.
⁸ Wale wapumbavu wakawaambia wenye busara, Tupeni mafuta yenu kidogo; maana taa zetu zinazimika.
⁹ Lakini wale wenye busara wakawajibu, wakisema, Sivyo; hayatatutosha sisi na ninyi; afadhali shikeni njia mwende kwa wauzao, mkajinunulie.
¹⁰ Na hao walipokuwa wakienda kununua, bwana arusi akaja, nao waliokuwa tayari wakaingia pamoja naye arusini; mlango ukafungwa.
¹¹ Halafu wakaja na wale wanawali wengine, wakasema, Bwana, Bwana, utufungulie.
¹² Akajibu akasema, Amin, nawaambia, siwajui ninyi.
¹³ Basi kesheni, kwa sababu hamwijui siku wala saa.

Usichoke kuuchochoea Moto wa Mungu kila iitwapo leo, jitoe kwa uaminifu mbele zake ili siku ile ya kuja kwake usije ukaachwa nyuma.

HITIMISHO:

Wapendwa katika Bwana tujitahidi kuishi kama watumishi wa Mungu.

Bali ninyi ni mzao mteule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu wa milki ya Mungu, mpate kuzitangaza fadhili zake yeye aliyewaita mtoke gizani mkaingie katika nuru yake ya ajabu; ninyi mliokuwa kwanza si taifa, bali sasa ni taifa la Mungu; mliokuwa hamkupata rehema, bali sasa mmepata rehema.
—1 Petro 2: 9-10 (Biblia Takatifu)

Nimefika tamati!

(Somo hili limefundishwa katika group letu la WhatsApp kwenye kipindi maalum cha Neno la Mungu, Tarehe 18/07/2019)