SIKU YA TATU YA SEMINA YA MAOMBI: Anawalisha Mch. Peter Sponger

mylogo20171203083016-2111862196.png

TOFAUTI KATI YA KUOMBA KUTAFUTA NA KUBISHA MBELE ZA BWANA:

Mwalimu wako akupendae ni mimi Mjakazi wa Bwana;

Mch. Peter Sponga.

DAY THREE SEMINAR 29/12/2017


Utangulizi:

Maombi ni sawa na kapu kubwa ambalo ndani yake kuna kuomba (ask) , kutafuta (search) na kubisha(to knock)
Mathayo 7:7 inasema; “ombeni nanyi mtapewa tafuteni nanyi mtaona bisheni nanyi mtafunguliwa”
Hapa Bwana Yesu alikuwa anaongelea vitu tofauti 3 ambavyo vyote vinapatikana katika nyumba inayoitwa MAOMBI na vyote vinafanyika mbele za Bwana zinaletwa na mwanadamu.

KUOMBA MBELE ZA BWANA:

KUOMBA ni kitendo cha kupeleka mahitaji, mashitaka, mapendekezo na shukrani mbele za Bwana. Yeremia 29:11-14… Ninawawazia mema……..mtaniita, mtaniomba nitawasikiliza……….
Aina Za Maombi:

  1. Maombi ya kufunga
  2. Maombi ya Vita
  3. Maombi ya Nadhiri
  4. Maombi ya mkesha
  5. Maombi ya mlimani

Mambo Ya Kufanya Wakati Unaomba:
Daniel 9:1-6, ….muelekee Bwana……ungama dhambi zako…….muinue Bwana…….Omba kwa bidii……Funga (acha kula na kunywa) ……vaa magunia (usijipambe), jipake majivu au jidhili, …lia mbele za Bwana , toa sadaka.
Unapoomba Kumbuka Mambo Haya:

  • Tunaomba kwa Imani. “Yesu akajibu, akawaambia, Amin, nawaambia Mkiwa na imani, msipokuwa na shaka, mtafanya si hilo la mtini tu, lakini hata mkiuambia mlima huu, Ng’oka, ukatupwe baharini, litatendeka. Na yo yote mtakayoyaomba katika sala mkiamini, mtapokea.” Mathayo 21:21-22.
  • Tunaomba bila kukoma. “ombeni bila kukoma;” 1 Wathesalonike 5:17
  • Tunaomba tukiwa tumejitakasa. “Jiosheni, jitakaseni; ondoeni uovu wa matendo yenu usiwe mbele za macho yangu; acheni kutenda mabaya; jifunzeni kutenda mema; takeni hukumu na haki; wasaidieni walioonewa; mpatieni yatima haki yake; mteteeni mjane. Haya, njoni, tusemezane, asema Bwana. Dhambi zenu zijapokuwa nyekundu sana, zitakuwa nyeupe kama theluji; zijapokuwa nyekundu kama bendera, zitakuwa kama sufu.” Isaya 1:16-18
  • Tunaomba tukiwa tunajua kuwa Bwana anatusikia. “Tazama, mkono wa Bwana haukupunguka, hata usiweze kuokoa wala sikio lake si zito, hata lisiweze kusikia;” Isaya 59:1

Maombi Yanauwezo Wa Kufanya Nini??

  1. Yanatupatia kibali. “Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa” Mathayo 7:7
  2. “ninyi nanyi mkisaidiana nasi kwa ajili yetu katika kuomba, ili, kwa sababu ya ile karama tupewayo sisi kwa msaada wa watu wengi, watu wengi watoe shukrani kwa ajili yetu” 2 Wakorintho 1:11
  3. “Maana najua ya kuwa haya yatanigeukia kuwa wokovu wangu, kwa sababu ya kuomba kwenu, na kuruzukiwa Roho wa Yesu Kristo” Wafilipi 1:19
  4. Hupunguza masumbufu. “Msijisumbue kwa neno lo lote; bali katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu.” Wafilipi 4:6
  5. “kwa kuwa kimetakaswa kwa neno la Mungu na kwa kuomba” 1 Timotheo 4:5
  6. “Ungameni dhambi zenu ninyi kwa ninyi, na kuombeana, mpate kuponywa. Kuomba kwake mwenye haki kwafaa sana, akiomba kwa bidii” Yakobo 5:16.

Kwa hiyo maombi ndio Bomu ya nyuklia hata leo katika ulimwengu wa Roho linaweza kufanya mengi ambayo hujawahi ona au kusikia kama ulikuwa unalega lega anza upya, boresha uwezo wako wa kuomba, ongeza muda nawe utaona matokeo makubwa ubarikiwe sana.
Nguvu Ya Kuomba Inatoka Wapi?

  • Kwa Roho mtakatifu; “Kadhalika Roho naye hutusaidia udhaifu wetu, kwa maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo, lakini Roho mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa.” Warumi 8 :26
  • Kwa kutubu vema. “Ikiwa, watu wangu, walioitwa kwa jina langu, watajinyenyekesha, na kuomba, na kunitafuta uso, na kuziacha njia zao mbaya, basi nitasikia toka mbinguni na kuwasamehe dhambi yao, na kuiponya nchi yao.” 2 Nyakati 7:14
  • Ahadi Mungu alizoahidi kwa vinywa vya watumishi wake. “Niite, nami nitakuitikia, nami nitakuonyesha mambo makubwa, magumu usiyoyajua.” Yeremia 33:3
  • Katika Neno. “Tena ipokeeni chapeo ya wokovu, na upanga wa Roho ambao ni neno la Mungu;” Waefeso 6:17

Mambo Ya Tahadhari Ni Kuwa Unapoenda Kuomba:

  • MUNGU NI SHAHIDi; “Naona uso wa baba yenu, kwamba hanitazami vema kama jana na juzi. Lakini Mungu wa baba yangu amekuwa pamoja nami.” Mwanzo 31:5
  • MUNGU NI MKUU; “Tazama, nitakujibu, katika neno hili huna haki; Kwa maana Mungu ni mkuu kuliko mwanadamu.” Ayubu 33:12
  • MUNGU NI MWAMUZI WA HAKI; “Mungu ni mwamuzi mwenye haki, Naam, Mungu aghadhibikaye kila siku.” Zaburi 7:11
  • MUNGU NI MWAMINIFU; “Mungu ni mwaminifu ambaye mliitwa na yeye mwingie katika ushirika wa Mwanawe, Yesu Kristo Bwana wetu.” 1 Wakorintho 1:9; “Jaribu halikuwapata ninyi, isipokuwa lililo kawaida ya wanadamu; ila Mungu ni mwaminifu; ambaye hatawaacha mjaribiwe kupita mwezavyo; lakini pamoja na lile jaribu atafanya na mlango wa kutokea, ili mweze kustahimili.” 1 Wakorintho 10:13
  • MUNGU YUPO PATAKATIFU; “Magari ya Mungu ni ishirini elfu, maelfu maelfu; Bwana yumo kati yao kama katika Sinai, Katika patakatifu.” Zaburi 68:17
  • MUNGU NI HAKIKA NA YUPO; “Lakini pasipo imani haiwezekani kumpendeza; kwa maana mtu amwendeaye Mungu lazima aamini kwamba yeye yuko, na kwamba huwapa thawabu wale wamtafutao.” Waebrania 11:6
  • MUNGU NI ROHO; “Mungu ni Roho, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli.” Yohana 4:24

Ukijua siri hii maombi yako yatajibiwa kila mara nawe utapata raha katika maisha ya wokovu na utumishi.

KUTAFUTA MBELE ZA BWANA

Ezra 4:19 nikatafuta habari na kugundua……
Kutafuta mbele za Bwana ni kuchunguza, ni kutaka kujua, au kutafuta tafsiri au sababu au mahali kuhusu jambo fulani lililofichwa.
Samweli 23:22, 23…. mkazidi kupata uhakika mkajue na kuona….Anapojificha……..Chunguzeni mkayajue maficho…..
Maombi ya kutafuta mbele za Bwana ni;

  • Maombi ya kuchimbua hazina zilizofichwa.
  • Maombi ya mafunuo, yanayoleta maono mapya ni yakugusa na kuleta visivyoonekana.
  • Maombi ya kudhibitisha na kuweka vitu hadharani.
  • Maombi yanayoumba imani kuwa kweli.
  • Si maombi ya kushitaki kupeleka mahitaji, siya wakati wa shida.
  • Maombi ya kuhitaji ufafanuzi

Tunawezaje Kumtafuta Bwana???

  1. Kusoma maandiko Ezra 6:1
  2. Kutumika nyumbani mwake.
  3. Kuondoa miungu na sanamu na kumuweka yeye namba moja. 2Nyak34:3… Yosia alimtafuta Bwana kwa kuondoa miungu na sanamu na maashera katika ufalme wake familia na kwa wote wanaomuhusu.
  4. Kwa kueneza injili ni huko ambako Mungu hujifunua na kutenda makuu. Jenga madhabahu kila unakoenda; ofisini, jenga madhabahu ikifika wakati fulani mtafute Bwana nyumbani, Dukani nk… Daniel alijenga madhabahu nyumbani, Dan 6:10
  5. Kushiriki kujenga hekalu la Bwana 1Nyak 22:19

Kwanini Tumtafute???

  • kwa sababu amesema tumtafute

Anataka kujitambulisha kama mwenye uweza kila mara katika jambo tofauti kumbuka misri alipiga mapigo kumi wakati moja lingetosha

  • Anataka kutufanikisha – 2Nyakati 26:5

Utafutaji huwa ni kwaajili ya vizazi vingi simeoni alishinda hekaluni na kulala humo kutafuta kumuona mwokozi wa ulimwengu. Luka2: 26-32, Ezra 8:21, 22

  • Ili mkono wake uwe juu yetu ututendee mema. Ezra 8:22
  • Ili tuponywe na hofu zote. Zab 34:4-10

Maombi haya ni ya level ya juu maombi haya ni ya watu ambao wameamua maisha yao yawe ya maombi. Maombi haya huja na unabii, mafunuo hufichua dhambi za siri.
Ezra aliomba sana maombi haya angalia ezra 8:22…. tuliona haya kumuomba mfalme tukafunga na kumsihi (kutafuta kama upo msaada)….. Bwana akatutakabali.

KUBISHA MBELE ZA BWANA:

Maombi ya kubisha au kugonga mlango ni maombi ya kumsihi Bwana kughairi mipango yake, hasira yake, juu yako au juu ya taifa. Maombi haya ni maombi ya kuomba upendeleo kuomba yasiyo ya haki yako. Unaweza ukayaita maombi ya toba au rehema.
2 samweli 24: 12, 16, 24-25
Mungu anakuwa amesha sema itakuwa hivi unaingia kuomba aghairi alikuwa amefunga mlango unaomba afungue. Daudi aliombana tauni ikakoma.
Maombi haya ni maombi ambayo unajua ukweli kuhusu jambo halafu unaomba upendeleo. Paulo na Barnaba wanashuhudia kuwa mlango kwa mataifa mliokuwa mnabisha nao umefungiliwa. Matendo 14:26-28
KUMBUKA:Mara nyingi tunabisha mlangoni. Katika ulimwengu wa Roho. Mlango ni kizuizi chochote kinachozuia mpenyo, mafanikio, wewe kuona, kuvuka nk
Kwahiyo milango ni mila, sheria, tamaduni, umri, jinsia, kabila, mazingira, asili nk. Ili ujue mlango ulikuwa umefungwa angalia majibizano kati ya Bwana na Petro kwaajili ya Kornelio. Mdo.10:9-16. Angalia Petro alivyokuwa anasuasua na namna Roho mtakatifu alivyoshuka hata kabla hajaomba
Mdo 10: 34-37…. Petro anasema hakika Mungu hana upendeleo bali katika kila taifa, dhehebu, kabila, jinsia, lugha; amchaye Bwana na kutenda haki atakubaliwa naye.
Inamaanisha ukibisha yale wengine wanafanya katika ufalme huu wa Mungu na wewe waweza kufanya maana Mungu wetu ni Mungu wa yasiyowezekana. Kornelio milango ilikuwa imefungwa lakini kupitia maombi haya mpenyo ulipatikana.
Angalia Matendo 10:1-4….. Kwa uchaji wa Mungu, utaua, kujidhiri cheo chake, kwa kutoa sadaka nyingi maana yake ziada, kuomba daima, akaona yaani kizuizi kikaondoka maono waziwazi… sala zako na sadaka zako zimefika.
Mungu awabariki kwa somo hili muwe na muda mzuri, hakika tukijua wakati gani ni wa KUOMBA wakati gani wa KUTAFUTA na ni wakati gani wa KUBISHA; hapo ndipo tutatenda kama Yesu na makubwa kuliko yale

Amen utukufu kwa Bwana; tuzidi katika kuombeana!

Mjakazi mtiifu kwa Bwana Yesu

Pastor Peter Sponga

Bahi Dodoma Tanzania

Chief Admin Jesus Co-Workers Ministry

YouTube: pastor peter sponga